Njombe waanzisha benki

ramani ya mkoa wa Iringa
WILAYA ya Njombe imepongezwa kwa kuanzisha Benki ya Wananchi (Njocoba) ili kukuza uchumi na kuongeza mtaji kwa wananchi. Pongezi hizo zilitolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Dk Mohamed Gharib Bilal alipokuwa akizungumza na wananchi baada ya kuzindua benki hiyo wilayani Njombe.
“Njombe mmeamua kukuza uchumi kwa kutanua fursa za kibenki,” alisema Dk Bilal.Alisema uamuzi huo umekuja wakati muafaka wakati serikali ikiendelea kuimarisha ushirikiano baina yake na sekta binafsi.
Alisema baada ya Njombe kuwa mkoa mpya, benki ni taasisi muhimu kwa kuwa itajenga misingi ya kifedha na kiuchumi.
Makamu wa Rais, ameitaka benki ya wananchi Njombe kutoa hamasa kwa wakulima wengi kuendeleza kilimo ili kukuza uchumi.Akizungumzia ushindani katika soko la kifedha na benki, aliitaka taasisi hiyo kuwajibika na kutoa taarifa kwa umma ili kukabiliana na hali hiyo.
“ Njombe ipo katika ushindani mkubwa na benki za biashara, hivyo hakikisheni mnarejea katika uwazi, ukweli na uwajibikaji na kutoa taarifa kwa umma,” alisema.
Aliitaka benki hiyo kuwa darasa katika maeneo mengine ili waijifunze jinsi ya kuendesha benki ya wananchi. Dk Bilal aliwataka wafanyakazi wa benki hiyo kufanya kazi kwa kuwaheshimu wateja na kuwachangamkia ili wawe karibu na benki hiyo.
Akizungumzia uhusiano wa benki na wananchi masikini, Makamu wa Rais aliitaka benki hiyo kubuni huduma nafuu kwa wananchi masikini ili nao waone kuwa ni sehemu ya benki hiyo. Makamu wa Rais yupo katika siku ya pili ya ziara yake ya kiserikali katika mkoa wa Iringa.







